UJINGA WA FISI KATIKA KUTATUA TATIZO LA KUKOSA AJIRA.


Ujinga wa fisi ni zile hesabu zake za kujidanganya. Akimuona binadamu anatembea, yeye anamfuata nyuma anamvizia. Jinsi binadamu anavyotembea kwa kutupa mikono, fisi anaamini kuwa muda wowote utadondoka kisha yeye ataubeba kwendaa kuufanya kitoweo.

Fisi anabaki kuwa mnyama mjinga kwa sababu mkono wa binadamu haudondoki. Siku fisi atakapojua kuwa binadamu kutupa mikono ndiyo kutembea kwake hatakuwa mjinga tena, ataacha kumfukuzia.
Katika soko la ajira, unapoiga ujinga huo wa fisi kisha wewe ukajiongeza kiakili, unaweza kujikuta unapata matokeo makubwa yenye kutimiza ndoto zako. Muhimu ni nidhamu na udhamirie kweli.
Unawezaje kuutumia ujinga wa fisi kufanikiwa? Jibu lake linakuja na swali, je, wewe unapenda kufanya kazi gani? Jawabu lako ndilo linaweza kukuongoza kutambua mahali ambako unapaswa kupawinda mithili ya fisi kwa binadamu.
Vema kufahamu kuwa ajira ni ngumu lakini wakati huohuo zipo ndoto ambazo wewe unaweza kuwa nazo. Mahali ambako unaona panaweza kutimiza ndoto na malengo yako ndipo unapotakiwa kupawinda kadiri inavyotakiwa.
Njia muhimu ya uwindaji wako ni kujiweka karibu na taasisi ambayo wewe unailenga kuifanyia kazi. Taasisi ya ndoto zako, itakayokufanya ujione ndoto zako zimetimia kama utafanikiwa.
Unawezaje kuiwinda? Jibu rahisi. Ni kwamba unafahamu kuwa kwenye taasisi hiyo eneo ambalo ungependa kulifanyia kazi limejaa. Kwa hiyo unaamua kujipeleka au kujipitisha mara kwa mara ukitumia sababu tofauti kusudi ukutane na bahati yako siku moja.
Mbali na kujipitisha unaweza kuomba kazi ya kiwango cha chini ambayo ni rahisi kupewa, baada ya hapo unaamua kujipambanua uwezo wako kuhusiana na kitengo cha ndoto zako. Hakikisha unabaki wewe na ndoto zako, usibadilishwe na hiyo kazi ambayo utakuwa umeiomba kama chambo cha kuifikia kazi ya ndoto zako.
Mathalan, unatamani kuwa ofisa masoko wa taasisi fulani lakini nafasi hakuna. Unaamua kuingia kazini na kuomba upewe kitengo cha usafi. Wakati ukitumikia eneo lako la usafi, unakuwa unajiweka wazi kuhusu uwezo wako wa masoko.
Kwa vile tayari upo ndani na uwezo wako unafahamika, inakuwa rahisi siku idara ya masoko ikikumbwa na upungufu, wewe unaitwa kuziba pengo, hivyo kutimiza ndoto zako. Hiyo ndiyo mbinu ya kuuiga ujinga wa fisi kwa kutumia akili.
Una ndoto kubwa za kuwa mhasibu mkuu kwenye taasisi kubwa unayoipenda na kuiamini, lakini nafasi ya uhasibu hakuna, kwa hiyo unaingia kazini kwa kuomba kazi ya utarishi (messenger), na wakati unatumikia nafasi hiyo unaonesha uwezo wako wa kihasibu.
Unakuwa ‘mesenja’ kwa kufanya kazi nzuri yenye kuvutia. Wakati ukiwa tarishi, unatumia mbinu mbalimbali kuuonesha uongozi kuwa wewe ni mhasibu mzuri. Siku idara ya uhasibu ikikumbwa na upungufu, wewe unapewa kiti.
Unataka kuwa dereva wa kampuni lakini madereva wamejaa tele. Unaamua kuingia kazini kama fundi magari, unafanya kazi nzuri huku ukionesha ni kwa kiasi gani ulivyo dereva bora. Siku upungufu wa madereva ukitokea wewe unaula.
Njia hii inahitaji nidhamu, kujishusha na uvumilivu. Maana upo kwenye mtego ukiwa hujui huo upungufu utatokea lini. Usipokuwa na subira ni rahisi kukata tamaa. Ila wapo walioamua kusubiri na matokeo waliyapata.
Larry King na ufagizi redioni
Mtangazaji Larry King ni mmoja kati ya watangazaji wenye mafanikio makubwa zaidi duniani. Mafanikio ya Larry yanagusa maeneo yote matatu katika maisha ya binadamu; umaarufu, heshima na utajiri.
Larry ambaye jina lake halisi ni Lawrence Harvey Zerger, anabaki kuwa mmoja wa waendesha mahojiano bora ya moja kwa moja kwenye televisheni, akiwa na rekodi ya kuwahoji watu wengi mashuhuri ulimwenguni, ikiwemo wanasiasa, wasanii na wanamichezo.
Kipindi chake cha Larry King Live kilichokuwa kinarushwa kwenye televisheni ya CNN, kiliweka rekodi ya kuendesha mahojiano na kila mtu maarufu ambaye watu wangependa kumsikia, yeye alimwalika na kumhoji.
Larry na mafanikio yake, alipata kusema kuwa katika maisha yake ya kikazi ametosheka mno kwa mahojiano, anasema watu wawili ambao wanamuuma hajapata nafasi ya kuwahoji ni Yesu na Rais wa 16 wa Marekani, Abraham Lincoln ambao walikuwepo na kuondoka duniani miaka mingi kabla yake.
Safari ya Larry kufikia mafanikio hayo yalianzia kwenye ufagizi wa redio. Alitamani kuwa mtangazaji lakini vipindi vyote vilikuwa na watu, kwa hiyo yeye akaomba nafasi ya kuwa mfagiaji wa studio na kusafisha vifaa vingine vya kurushia matangazo.
Larry ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 82, hakwenda chuo kwa sababu ya uwezo duni wa kifamilia. Baba yake alifariki dunia mapema, mama yake akawa anaishi kwa akutegemea fedha za kujikimu kutoka serikalini.
Mwaka 1950, Larry alikutana na mtangazaji mmoja wa Radio CBC kama bahati. Mtangazaji huyo baada ya kuiona kiu ya Larry kuwa mtangazaji, alimshauri aende Jimbo la Florida kwa sababu wakati huo kulikuwa na uchipuaji wa vituo vya matangazo ya redio, hivyo kupata kazi ilikuwa rahisi.
Larry aliwasili jijini Miami, Florida na baada ya kuhangaika sana kutafuta ajira ya utangazaji bila mafanikio, alijiunga na Radio WAHR ambayo siku hizi inaitwa WMBM kwa kazi ya kufagia na kusafisha vifaa vya studio.
Alifanya kazi hiyo kwa nguvu zote, kila siku alikuwepo kazini. Katika kujiongezea thamani akawa anajipenyeza na kushauri masuala mbalimbali ya utangazaji na uandaaji wa vipindi.
Mei Mosi, 1957, mtangazaji wa kipindi cha asubuhi saa 3 mpaka 6 mchana aliacha kazi. Meneja Mkuu wa WAHR, Marshall Simmonds akamwamaini Larry aongoze kipindi hicho kama DJ, muziki na mazungumzo. Kuanzia hapo maisha ya Larry yalianza kubadilika.
Alichofanya Larry ni kubadili uelekeo mara kwa mara. Matokeo yake Larry akafika CNN, mara akawa mwendesha mahojiano anayeogopwa zaidi na viongozi wakubwa ulimwenguni.
Larry alijipenyeza WAHR kama mfagiaji na maisha yamekuwa mazuri upande wake. Ndoto zimetimia. Hata sasa, Larry anaendelea kutengeneza fedha kupitia vipindi vyake vya Larry King Now na Politicking with Larry King ambavyo vinarushwa hewani na chaneli za televisheni za Marekani, Hulu na RT America.
Unafahamu kuhusu Gardner Habash?
Gardner Gabriel Habash ni mtangazaji maarufu nchini na ambaye inaaminika ni mmoja wa watangazaji wenye kulipwa fedha nyingi zaidi kwa sasa. Kwa wakati huu, anatumikia ajira yake Redio Clouds Fm.
Siku moja Gardner aliwahi kutoa ushuhuda kuwa alikwenda Clouds Fm kuomba kazi ya uofisa masoko lakini baadaye Mkurugenzi wa Vipindi, Clouds Media Group alimbadilishia kazi, akampa utangazaji ambao ameng’ara nao na kumfanya ajisifu kuwa ametimiza ndoto zake.

BONYEZA HAPA ?UJIPATIE KITABU CHA JINSI YA KUTENGENEZAJI WA BIDHAA MBALIMBALI ZA VIWANDANI KAMA sabuni ya mche, sabuni ya unga, ya maji, batiki n.k

Imetolewa na 
Mwl.  Pius Justus Muliriye 
0754745798 /0657128567 
piusjustus28@gmail.com 

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *