Vijana hao walienda pembeni mwa mji, ambako kulikuwa na na msitu. Wakiwa mule porini wakifanya zoezi la kutafuta mafanikio walikutana na ajuza mmoja. Yule ajuza aliwauliza, “Mnatafuta nini wajukuu zangu huku porini?”
“Tunataka utajiri bibi” alijibu mmoja wa wale vijana. Yule bibi aliwaonesha jiwe kubwa sana, akawaambia chini ya hilo jiwe kumefichwa utajiri mkubwa sana.
Wale vijana walikwenda hadi kwenye jiwe hilo. Walipofika, waliingia kwenye pango kubwa lililokuwapo chini ya lile jiwe. Walipoingia ndani, kulikuwa na giza totoro. Wakamulika kwa tochi na kutazama ndani waliona vitu viking’aa! Loh, yalikuwa ni madini ya thamani kubwa sana ulimwenguni.
Walianza kushangilia kwa furaha kubwa kwakuwa ndoto zao za kuwa mabilionea zimetimia. Hatimaye wakaanza kujadili namna ya kuyabeba yale madini. Wakafikia muafaka kwamba, wamtume mmoja wao aende mjini akanunue mabegi matatu kulingana na idadi yao ili waje wabebee yale madini. Hivyo, walimpatia mmoja wao kipande kidogo cha almasi ili akauze apate fedha ya kununua mabegi.
Baada ya kijana huyo kuondoka kwenda mjini kwa ajili ya kununua mabegi, wale jamaa wawili waliobaki pale pangoni walianza kujadili namna ambayo wanaweza kufanya ili wamdhulumu yule jamaa madini. Unataka kujua nini walichopanga? Ntakwambia. Walipanga wamuue pindi tu atakapokuja ili waitumie ile fursa kumiliki yale madini yote wao wenyewe.
Baada ya muda mrefu yule jamaa alikuja, ukiwa ni usiku kwakuwa mjini kulikuwa mbali. Alipofika tu mule pangoni, wale jamaa wawili walimvamia na kumshambulia hadi wakamuua! Walipokamilisha zoezi hilo, wakaanza kufanya mpango wa kubeba madini yale.
Wakati wanafungua yale mabegi, walikuta chakula. Wakafurahi kwakuwa walikuwa na njaa sana. walikula kile chakula hatimaye wakamaliza na kuanza kupakia madini kwenye mabegi. Hazikupita dakika nyingi wakaanza kuumwa matumbo vibaya! Hatimaye walikufa kwakuwa walikula chakula chenye sumu kali ambayo iliwekwa na marehemu rafiki yao kwa ajili ya kuwaangamiza ili amiliki madini yote peke yake.
Umejifunza hapo ni nini kilichokosekana kwa hawa jamaa? Bila shaka ni kile alichokisema Bwana Zig Zigler, “Unaweza kupata kila kitu unachohitaji endapo utawasaidia watu wengi zaidi wapate kile wanachohitaji” Hii ni sawa na kusema kwamba; uwezo wako wa kufanikiwa unatokana na uwezo wako wa kutatua matatizo ya watu. Uwe mtu wa kuleta majibu na suluhisho.
Hawa jamaa walifanya kinyume! Matokeo yake hawajafanikiwa kufika popote, wakaangamia. Ndivyo ilivyo kwa watu wengi. Wamejawa na choyo! Hawapendi kuona wengine wanafanikiwa. Nadhani hawafahamu kwamba hakuna anayefanikiwa peke yake. Lazima awe na watu ambao watakuwa sehemu ya mafanikio yake.
Hebu rafiki yangu uwe suluhisho la matatizo ya watu. Utaona mafanikio yanavyokuja hadi utashangaa. Dunia ina changamoto nyingi sana! naamani ungezingatia sana kauli hii, ngoja niirudie; Duniani kuna changamoto nyingi sana. wanaofanikiwa kuleta suluhisho wanakuwa na mafanikio makubwa sana. ndio wanaotamba! Leo hii unatumia hicho kifaa kusoma makala hii, tambua kuna alijua kwamba hilo ni hitaji. Hivyo akaamua kuwasaidia watu waweze kuondokana na changamoto hiyo.
Sasa inawezekana wewe huna maono makubwa sana ya kutatua matatizo katika ukubwa wa dunia nzima, lakini angalia jamii yako inayokuzunguka ina matatizo gani? Kama kuna ukosefu wa maji, huwezi kuchimba kusima ukawa umeleta suluhu? Kama kuna ukosefu wa mboga za majani na matunda, huwezi kulima bustani? Kama kuna ukosefu wa nyama na mayai huwezi kufuga kuku ukawasaidia kuimarisha upatikanaji wa mayai?