Ualimu ni moja ya taaluma muhimu sana kwenye jamii yoyote. Walimu ndiyo wanaoijenga jamii kutokana na malezi wanayotoa kwa watoto ambao ni kizazi kinachokuja.
Pamoja na umuhimu huu mkubwa wa taaluma ya ualimu, maslahi yamekuwa siyo mazuri. Walimu wamekuwa ndiyo watu wa kulalamika kila siku kuhusu mishahara midogo na kutokuendana na gharama za maisha. Hapo bado hujaangalia wale ambao wamehitimu taaluma hii lakini hawakupata kazi.
Kauli za viongozi wengi zimekuwa ni kwamba kama umekosa kazi au kama kipato hakikutoshi basi jiajiri. Lakini walimu wengi wamekuwa wakilalamika kwamba wao wanawezaje kujiajiri kwa taaluma yao? Mtu atawezaje kwenda kuanzisha shule yake binafsi wakati hana kazi kabisa, au mshahara wake haumtoshi?
Njia rahisi ya kujiajiri au kujiongezea kipato iliyokuwa imezoeleka na walimu ilikuwa kutoa masomo ya ziada kwa wanafunzi maarufu kama tuition, lakini hii pia imepigwa marufuku maeneo ya shuleni.
Hali kama hizi zinawafanya walimu wajione hawawezi kuondoka kwenye matatizo waliyopo. Lakini leo nataka kuzungumza na kila mwalimu ya kwamba ipo njia rahisi ya wewe kujiajiri, itakayokuwezesha kutengeneza kipato cha ziada, bila ya kuacha kile unachofanya sasa.
Njia hii ni kujiajiri na kutoa huduma kupitia mtandao wa intaneti.
Sasa hivi karibu kila mtu mwenye simu anatumia mtandao wa intaneti, na namba inazidi kuongezeka kila mwaka. Hivyo walimu wanaweza kutumia mtandao huu wa intaneti kuweza kutoa huduma kwa wale wenye uhitaji, na baadaye wakaweza kutengeneza kipato.
Kwenye mtandao wa intaneti, unatoa maarifa na taarifa zinazowasaidia watu kufanya maamuzi bora kabisa ya maisha yao.
Kabla ya kuangalia mwalimu anawezaje kutengeneza fedha kwenye mtandao wa intaneti, kwanza soma vitu vitatu muhimu unavyohitaji kuwa navyo ili kutengeneza fedha kwenye intaneti. Visome kwa kubonyeza maandishi haya.
Zifuatazo ni njia kumi(10) anazoweza kutumia mwalimu kutengeneza fedha kwenye mtandao wa intaneti.
Zifuatazo ni njia kumi(10) anazoweza kutumia mwalimu kutengeneza fedha kwenye mtandao wa intaneti.
- Kuandika makala zinazohusu elimu kwa ujumla. Hapa itakuwezesha kujijenga kama mtaalamu wa elimu na hivyo kupata fursa zaidi za kushauri na kufundisha kuhusu elimu.
- Kuuza vifaa vya ufundishaji ambavyo umetengeneza au kuandaa mwenyewe. Kama mwalimu unaweza kuwa na notes nzuri ulizoandaa, maswali mazuri na vitu vingine vinavyoweza kutumika kufundisha.Unaweza kuzitengeneza vizuri na kuziuza kupitia mtandao wa intaneti.
- Kuandika kuhusu malezi ya watoto. Moja ya vitu ambavyo walimu wanajifunza ni malezi, kitu ambacho wazazi wengi hawajajifunza. Hivyo mwalimu anaweza kuwa anatoa mafunzo ya aina hii na baadaye kuwa mshauri au kutoa mafunzo ya kulipia juu ya malezi bora ya watoto.
- Kupata fursa ya kufundisha watoto masomo ya ziada majumbani kwao. Kwa kuwa tuition mashuleni zimekatazwa, mwalimu anaweza kutoa masomo ya ziada kwa kuwafuata wanafunzi kule walipo. Kwa kutumia mtandao wa intaneti, mwalimu anaweza kuwafikia wateja wake wa huduma ya masomo ya ziada.
- Kuandaa kozi utakayoitoa kwa njia ya mtandao. Kupitia mtandao wa intaneti, mwalimu anaweza kuandaa na kutoa kozi ambayo watu watajiandikisha na kulipia. Kozi hii inaweza kuhusu mambo mbalimbali yanayoweza kuwasaidia watu.
- Kuandika kitabu na kukiuza kwa njia ya mtandao. Kitabu hiki unaweza kukichapa au kukiuza kama nakala tete kama ambavyo ninafanya mimi, ninaandika vitabu mbalimbali na kuviuza mtandaoni.
- Kutoa ushauri na mafunzo kwa walimu waliopo vyuoni bado, namna bora ya kusoma na kufaulu mitihani, mambo muhimu ya kuzingatia wanapoanza kazi na hata namna ya kuendeleza na kukuza taaluma zao.
- Kuandaa mtaala unaoweza kutumiwa na watu wanaolenga kutoa mafunzo fulani. Kama mwalimu una uzoefu juu ya mitaala, unaweza kutumia uzoefu huo kusaidia wengine wanaoanza kutoa mafunzo mbalimbali.
- Kutumia vipaji na uwezo ulionao kutengeneza fedha kwenye mtandao. Hapa unaweza kuandika au kufundisha juu ya vitu vingine unavyojua, ulivyozoea au unavyopenda nje ya ualimu.
- Kutumia mtandao wa intaneti kutangaza na kukuza biashara zako nyingine ulizonazo tayari. Kama tayari umeshaanza biashara nyingine, unaweza kutumia mtandao wa intaneti kuzikuza zaidi.
Wakati wa kulalamika kwamba wewe kama mwalimu huna njia za kuongeza kipato zimepitwa na wakati. Una taaluma muhimu sana na zipo njia za bure kabisa kwako kuzitumia kuweza kutengeneza fedha kwa taaluma uliyonayo. Anza kufanyia kazi hayo niliyokushirikisha, na kama utapenda ushauri wangu wa karibu zaidi na hata kukuongoza kwenye hilo, nitafurahi sana kufanya kazi na wewe. Tuwasiliane kwa njia ya wasap namba 0754745798. Karibu sana.
Tumia ujuzi, utaalamu na uzoefu wako kutengeneza kipato kwenye mtandao wa intaneti kupitia SHULE TANZANIA
PIUS J. MULIRIYE
Kocha wa mafanikio, Mwandishi na Mjasiriamali.
Karibu sana kwenye SHULE TANZANIA uweze kutengeneza kipato kupitia mtandao wa intaneti.