KUBALI WAJIBU BINAFSI

Natumaini umekuwa na siku njema kwako;




Napenda nikushirikishe makala hii ambayo itakupatia nafasi ya kujikumbusha na kujifunza mambo yatakayoongeza thamani maishani mwako.

Kuna siku nilikuwa napita barabarani maeneo ya stendi ya mabasi, nikamwona kijana mmoja akisukuma toroli lililosheheni mizigo. Bila shaka alikuwa kazini kwenye ajira yake akitoa huduma ya kuwabebea watu mizigo ili apate riziki aweze kusukuma mbele gurudumu la maisha yake na familia yake.

Nilichogundua ni kwamba; aliifanya ile kazi, lakini hakuipenda hata kidogo. Nilijuaje kwamba hakuipenda? Nilisikia maneno yake katika mazungumzo na rafiki yake.

Ilikuwa wakati akisukuma ule mkokoteni kwa nguvu, nilimsikia jamaa mmoja aliyekuwa ng’ambo ya pili akimwita kwa jina huyo jamaa anayehenya na mkokoteni, japo jina silikumbuki.
“Naona unakula shuluba mwanangu” alisema yule jamaa aliyekuwa ng’ambo ya barabara akimwambia yule anayesukuma toroli kwa sauti ya juu sana.

“Nakula msoto mwana. Ila namlaumu sana maza, angechagua baba mwenye hela haya yote yasingenikuta. Ningekuwa nakula hata tu!” alieleza yule msukuma toroli.

Kwanini nimetoa kisa hiki?, kuna kitu kikubwa cha kujifunza hapo. Watu wengi sana hapa duniani wanaishi maisha kama wahanga, wakiamini kwamba kuna watu wengine ndio waliowasababishia hali walizonazo na maisha wanayoyapitia. Licha ya kulaumu watu, wanalaumu hata mazingira, viongozi, taasisi, wanalaumu kila kitu. Wengine wanamlaumu hata Mungu wao! Wanadhani kwamba, huko ndiko matatizo yao yanakotokea.

Hawaelewi au wamesahau kwamba, chanzo cha hayo yote ni wao wenyewe. Kurusha lawama kwa wengine ni kukwepa wajibu binafsi na kuanza kutazama mazingira ya nje kama chanzo. Mageuzi makubwa sana utakayoyafanya maishani mwako ni kukubali wajibu binafsi, uanze kuyatazama maisha yako ukijua kwamba wewe ndiye uliyeyafikisha hapo na ni wewe pekee unayeweza kuyanusuru!

Kwa kawaida mwanadamu alivyo huwa hapendi kubeba lawama au kuwajibika katika makosa au jambo ambalo limetokea lisilo sawa. Ila anapenda kubeba sifa endapo mambo mazuri yamefanyika.

Ulishawahi kukutana na mtu akaanza kukueleza kuhusiana na mgogoro uliojitokeza baina yake na mtu mwingine? Je, mtu huyo alisema kwamba yeye ndiye chanzo cha yote na ndiye aliyekosea?

Mara nyingi hata kama mtu alikosea yeye, bado atarusha lawama upande wa pili kwamba ndiyo chanzo cha matatizo. Hawataki kubeba wajibu binafsi kuona kwamba wao ndio wanaohusika!

Endapo kila mtu angekuwa anabeba wajibu binafsi, familia zisingeyumba, biashara zisingedorola, watu wangeweza kuishi maisha yenye mafanikio wanayoyataka, watu wasingekuwa wanaenda kwenye kazi wasizozipenda zinazowapa msongo wa mawazo na homa, kubwa zaidi, kwa maoni yangu, dunia ingegeuka paradiso ndogo!.

SOMA: Ndoto yako ni ipi?

Siku ukiachana na kulaumu mazingira ya nje na kuangalia wajibu ulionao kuleta suluhu utashangaa kila kitu kitabadilika maishani mwako. Wakati wengine wanalalamika jua kali, wewe utaona fursa ya kutengeneza mwamvuli na kuwauzia.

#UNAWEZA
“Hakuna aliyefaulu kujenga maisha chanya kwa mtazamo hasi.”

SOMA: Uvivu wako wa kufikiri ndio umaskini wako

Nikutakie utekelezaji mwema wa haya;
Asante kwa kuendelea kuwa na mimi mpaka hapa.

Wasiliana nasi;

Pius Justus Muliriye
0754745798-Whatsapp
0657128567
piusjustus@gmail.com

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *